Kilwa,
Naibu waziri ofisi ya
Rais TAMISEMI Mhe. George joseph Kakunda amesema serikali itawachukulia hatua
kali za kisheria walimu wakuu na wote ambao watabainika kutengeneza uhamisho bandia
kwa wanafunzi wa kike kwa dhumuni la kwenda kuwaozesha.
Ameyasema hayo alipokua akizungumza na baadhi
ya watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Kilwa waliojitokeza katika ukumbi wa
jumba la maendeleo mjini Kilwa masoko.
Naibu waziri amesema
wale wote ambao watabainika kushiriki katika udanganyifu au njia nyingine
yeyote ambayo itatumika kukatiza masomo kwa wasichana basi adhabu kali
itachukuliwa juu yao ikiwemo kifungo cha miaka thelathini jela.
Amesema kuna baadhi ya
wazazi wamekua wakishirikiana na walimu wakuu kutengeneza uhamisho ambao unaonyesha kua mwanafunzi
anahamia shule Fulani lakini mwisho wa siku anaenda kuozeshwa bila kufika kule
ambako uhamisho unaonyesha.
“Nasema wale wote ambao
watakutwa na hatia ya kukatisha masomo kwa wasichana kwa ajili ya kuwaozesha basi
kifungo cha miaka thelethini kitamuhusu kuanzia mzazi, mshenga, shekhe au padri
atakaefungisha ndoa hio na wale wote watakao enda katika sherehe hio watafungwa
miaka thelathini jela.” Alisema naibu waziri
Pia naibu waziri amezitaka
mahakama kuharakisha hukumu kwa wale wote ambao watakutwa na hatia ya kukatisha
masomo kwa kuwatia mimba wanafunzi.
Aidha naibu waziri
ameipongeza Halmashauri ya wilaya ya Kilwa chini ya Mkurugenzi wake Bw. Zablon Bugingo
Kwa kuibua na kusimamia miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo imekua na manufaa
na tija kwa wananchi.
Akihitimisha mazungumzo
hayo mkuu wa wilaya ya Kilwa Mh. Christopher Ngubiagai ameahidi kuyafanyia kazi
maagizo na ushauri alioutoa naibu waziri kwa kushirikiana na wataalamu
mbalimbali kutoka halmashauri ya wilaya
ya Kilwa.
Akiwa wilayani Kilwa niabu waziri alitembelea
miradi mbalimbali ya kimaendeleo ikiwemo mradi wa uoteshaji wa miche ya
mikorosho ya kisasa, mradi ambao unasimamiwa na halmashauri ya wilaya ya Kilwa.
Halmashauri ya wilaya ya Kilwa kwa kushirikiana na
watalamu mbalimbali inaotesha jumla ya miche milioni moja ya mikorosho ya
kisasa ambayo inatarajiwa kugawiwa bure kwa wakulima ikiwa ni njia ya kuongeza
uzalishaji wa zao hilo sambamba na
kuongeza pato la halmashauri.
Kwa sasa wilaya ya
Kilwa ina jumla ya mikorosho laki sita tu ambayo msimu wa 2016/2017 iliingiza
kiasi cha shilingi Bilioni kumi na tatu za kitanzania na halmashauri ilipata zaidi ya shilingi
milioni 220 baada ya mgawanyo.
![]() |
| Picha ikionyesha viriba vya kuoteshea miche ya korosho |
Sign up here with your email


ConversionConversion EmoticonEmoticon