LIGI SOKA DARAJA LA PILI, NAMUNGO FC YAICHAPA COSMO FC 1-0 MAKACHO AIBUKA SHUJAA.



 Mlandizi, kibaha

Timu ya soka ya Namungo Fc kutoka Kijiji cha Namungo, Kata ya Mbekenyela Wilaya ya Luangwa Mkoa wa Lindi jioni ya Jumatano Oktoba 18 imeifunga timu kongwe ya Cosmo Politan ya jijini Dar es Salaam kwa bao 1-0 kwenye mchezo wa Ligi Daraja la pili.

Katika mchezo huo uliopigwa kwenye uwanja wa JKT Ruvu Mabatini Mlandizi Mkoa wa Pwani, bao la pekee la washindi limefungwa na Mustapha Makacho kunako dakika ya 45 baada ya kona safi iliyochongwa na Hamis Enzimbali mpira uliopata msitu wa mabeki wa Cosmo na kipa wao Issa Kalembe na kujaa wavuni.

Mchezo huo uliochezeshwa na mwamuzi James Andrew kutoka Morogoro akisaidiwa na Respicious Dismass, Godruck Dismass na Kassim Safisha aliyekuwa mezani, ulijaa ufundi mwingi kutoka kwa wachezaji wa pande zote mbili walioweza kucheza mpira wa kasi, pasi za uhakika na kila aina ya ufundi.

Makocha Furgence Novatus wa Namungo na Salumu Kumbalatalu walifanya mabadiliko ya wachezaji kazaa kwa lengo la kupata matokeo mazuri zaidi lakini hata hivyo hayakuweza kubadiliaha sura ya mchezo pamoja na kila upande kucheza kwa kasi kubwa na ufundi wa hali ya juu.

Namongo iliwatoa Seleman Bwenzi na Fariq Simba nafasi zao zikachukuliwa na Gambaleku Matiku na Hamisi Mayanga, uoande Cosmo wamewapumzisha Maulid Jumanne, Seleman Shida na Stephano John nafasi zao zikichukuliwa na Musa Kipao, Ramadhan Yusuph na Hija Jumanne lakini hata hivyo hayakuweza kubadili Sura ya mchezo.




Credit - Omary Mngindo, Mlandizi, Kibaha, Pwani, Tanzania
Previous
Next Post »