LIGI DARAJA LA NNE YAENDELEA KURINDIMA KILWA.



Kilwa,

   Timu ya Kilwa youth soccer academy imeibuka na ushindi mwembamba wa goli moja kwa sifuri dhidi ya Tamofa  fc kutoka mji mkongwe wa kihistoria  Kilwa kisiwani ikiwa ni muendelezo wa ligi daraja la nne ngazi ya wilaya kituo cha masoko.

Mtanange  huo uliotawaliwa  na kasi ya hali ya juu umepigwa mapema  leo katika uwanja wa mwenge (Taifa) mjini Kilwa Masoko huku ukishuhudiwa na idadi kubwa ya wapenzi na  wadau wa soka wilayani  hapo.

Timu zote   zilionyesha umahiri wa hali ya juu kwa kucheza  mchezo wa kujiamini  na kushambuliana kwa zamu hali ambayo ilipelekea timu hizo ziende mapumziko zikiwa hazijaruhusu nyavu kutikiswa.

Zikiwa zimesalia takribani dakika kumi ta tano kumalizika kwa pambano hilo, Mwalimu wa Kilwa Youth soccer academy alifanya mabadiliko  ya kiufundi kwa kumtoa  mchezaji Nurdin Bakari na kumuingiza Mohamed Hafidhi  ambaye alifunga goli pekee katika mtanange huo katika dakika za lala salama .

Katika mechi ya ufunguzi wa ligi hio  iliyopigwa siku ya juma tano katika uwanja wa mwenge (Taifa) mjini Kilwa timu ya Ngome fc kutoka Kilwa masoko ilichoshana nguvu na Tamofa Fc kutoka Kilwa kisiwani kwa sare ya magoli mawili kwa mawili huku Mihina Fc wao wakitoka suluhu dhidi ya Al qaeda katika mtanage wa pili uliorindima siku ya Alhamisi.

Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea tena kesho kwa mchezo mmoja ambapo majira ya saa kumi jioni timu ya Kichanga chui Fc itakua uwanjani wakimenyana na Al qaeda Fc zote kutoka Mjini Kilwa Masoko.

Ligi daraja la nne ngazi ya wilaya, wilaya ya Kilwa inajumuisha jumla ya timu kumi na nne ambazo zimegawanywa katika vituo vitatu ambavyo ni Masoko, Njia nne na Somanga ambapo kituo cha masoko kina timu sita, njia nne timu nne na somanga timu nne.

Baada ya kukamilika kwa michezo yote ya makundi mshindi wa kwanza kutoka katika vituo vya njia nne na somanga watamenyana na washindi wa kwanza na wa pili kutoka kituo cha masoko ambapo timu mbili  zitakazo shinda zitakua zimefuzu kwenda ngazi ya mkoa.
 

Previous
Next Post »