HOSPITALI YA WILAYA YA KILWA YAKABIDHIWA JENGO LENYE THAMANI YA SHILINGI MIL.186



   Kilwa,     

  Mkuu wa wilaya ya Kilwa Mh. Christopher Ngubiagai amewataka wanainchi kutunza rasilimali ambazo mungu amewajaalia kwa manufaa yao ya sasa na vizazi vijavyo.

Amesema endapo rasilimali hizo zitatunzwa na kutengenezewa mikataba bora zitasaidia kusukuma gurudumu la maendeleo kutoka lilipo sasa na kufikia uchumi wa kati.

Hayo ameyasema katika hafla fupi ya makabidhiano ya jengo jipya la wodi ya kina mama ambao wanasubiria kujifungua (Mama Ngojea) katika Hospitali ya wilaya ya Kilwa (Kinyonga) ambalo limejengwa kwa msaada wa Kampuni ya Uchimbaji Gesi ya Pan African Energy yaliyofanyika katika viunga vya Hospitali hio mapema wiki hii.

Pia Mh. Ngubiagai amewaonya wavuvi ambao wanaendesha shughuli za uvuvi kwa kutumia zana ambazo zimezuiliwa ikiwemo mabomu kuacha mara moja kwani zinahatarisha maisha ya viumbe hai vinavyoishi baharini pamoja na mabomba ya gesi ambayo yapo chini ya bahari.
Mkuu wa wilaya ya Kilwa Mh. Christopher Ngubiagai akizungumza na wananchi waliojitokeza katika Hafla ya makabidhiano ya Jengo la wodi ya kina mama Hospitali ya wilaya ya kilwa (Kinyoga).

Aidha Mh. Ngubiagaiamemuagiza Mkurugenzi mtendaji kushirikiana na wataalamu kutoa elimu kwa wananchi juu ya faida za kujiunga na mifuko ya bima za afya ambayo itawasaidia kupata huduma za matibabu muda wowote, pia amemtaka kupata idadi ya wazee katika wilaya ya Kilwa ili waweze kutengenezewa vitambulisho ambavyo vitawaruhusu kupata huduma za afya bure. 

Awali akizungumza katika hafla hio Meneja uwajibikaji na huduma za kijamii Kampuni ya uchimbaji Gesi Pan African Energy Nd. Andrew Kashangaki ameishukuru Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa kwa ushirikiano ambao inaendelea kuutoa kwa kampuni hio na kuahidi kuendelea kushirikiana nao katika masuala mbalimbali ya kijamii.
Meneja uwajibikaji na huduma za kijamii Kampuni ya uchimbaji Gesi Pan African Energy Nd. Andrew Kashangaki (kulia) akimkabidhi Mkuu wa wilaya ya Kilwa mfano wa Funguo kuashiria kufunguliwa kwa jengo hilo, kutoka kushoto ni Kaimu Mkurugenzi(w)  Nd. Kaunda.

Akihitimisha hafla hio Mwenyekiti wa mji mdogo wa Kilwa Kivinje Bw.Mohamedi Peta amewashukuru Pan African Energy kwa msaada wao na kuomba kuendelea na moyo huo wa kujitolea Hospitalini hapo misaada mbalimbali ikiwemo vifaa tiba pamoja na Mashine ya Mionzi ( X-ray Machine) kwani iliyopo Hospitalini hapo ina matatizo ambayo yamepelekea kusimama kwa huduma za X-ray.

Jengo la Mama Ngojea limegharimu kiasi cha shilingi Milioni mia moja themanini na sita (Mil.186) mpaka kukamilika kwake na linauwezo wa kuchukua wakina mama zaidi ya 20 kwa wakati mmoja hali ambayo itasaidia kupunguza mlundikano katika wodi za wazazi hospitalini hapo pindi wanapo subiria kujifungua.
Muonekano wa jengo jipya la Wodi ya wazazi(Mama Ngojea) lililo jengwa kwa msaada wa Kampuni ya Uchimbaji Gesi ya Pan African Energy katika Hospitali ya Wilaya ya Kilwa ( picha zote na Ally Ruambo)


Previous
Next Post »