MBWEMBWE ZATAWALA KUELEKEA MCHEZO WA FAINALI MSHIKAMANO CUP



Zikiwa zimesalia siku tisa kuelekea mchezo wa fainali mashindano ya Mshikamano Cup kati ya Leceister City Fc dhidi ya Black Mob Fc (Makuzi) mbwembwe za viongozi na mashabiki wa mpira wilayani Kilwa zimeanza kutawala.

Kila timu inajinasibu kua itamaliza mchezo ndani ya dakika 90 kwa kuibamiza timu pinzani goli zisizo pungua tatu na kuendelea.

Akizungumza na mwandishi wetu Msemaji wa timu ya Black Mob Fc Bw. Shaweji Mamboya amesema timu yake ipo timamu kwa asilimia mia kuelekea mchezo wa fainali licha ya kua na majeruhi mmoja ambaye anasumbuliwa na matatizo ya nyonga lakini anaamini mpaka kufikia siku ya fainali atakua yuko vizuri kwakua amekwisha anza mazoezi mepesi.

”Timu iko vizuri kwa asilimia mia na tumejiandaa kukabiliana nao hao wapinzani wetu siku hiyo ya fainali licha ya kua mchezaji wetu Mohamedi Kituga kua na  maumivu ya nyonga, lakini nina imani mpaka kufikia siku ya mchezo atakua yuko vizuri kwa kua amekwiasha anza mazoezi mepesi mepesi.
Niwatoe tu wasiwasi wapenzi na mashabiki wa Black Mob Fc kua tutachukua ubingwa, Ng’ombe wawili na zawadi zingine zitabaki kivinje.”Alisema 

Bw. Mamboya amejinasibu kua ana imani na safu yake ya ulinzi kwani mpaka kufikia hatua ya robo fainali ilikua imeruhusu goli nne tu na kwa morali waliokua nayo wachezaji wake hususani safu ya washambuliaji anaamini kabisa kua watamaliza mchezo huo ndani ya dakika tisini kwa kumfunga Leceister city Fc goli 3 kwa nunge.

“Kwetu sisi mechi ya nusu  fainali ndio huwaga ngumu miaka yote lakini hatujawahi kumuacha mtu salama katika hatua ya fainali.” Alisisitiza Bw. Mamboya 

Kwa sasa timu hio inaendelea na kambi katika mji wa kilwa kivinje wakijiandaa kuwavaa mahasimu wao Leceister City huku wachezaji wao mahiri Okwi na Manyanya wakionekana kujifua zaidi ili kuimaliza Leceister City Fc katika mtanange huo wa fainali.
Wachezaji wa Black Mob Fc (Makuzi) wakiwa na nyuso za furaha baada ya ushindi.



Kwa upande wao mabingwa watetezi wa mashindano hayo Leicester City Fc wamesema wanataka kuudhihirishia umma kua hawakubahatisha kuchukua ubingwa msimu uliopita kwa kuchukua tena ubingwa msimu huu.

Wamesema wako vizuri na mchezaji wao aliepata majeraha ameanza mazoezi mepesi na leo wanaanza rasmi kambi kwa ajili ya maandalizi kuelekea katika mchezo wa  fainali siku ya tarehe 2.

Mmoja wa waanzilishi wa timu hiyo Bw. Hamisi almaarufu Udeze amesema  hawana shaka kabisa juu ya ubingwa kwani ana kikosi kizuri na safu bora ya washambuliaji ikiongozwa na mtu mwenye njaa ya magoli Mustafa Makacho.

“Kuhusu ubingwa hilo hatuna shaka nalo kabisa kwani nina kikosi imara ambacho kina uwezo wa kufanya chochote katika mda wowote 

Nadhani hata hao Black Mob vichwa vitakua vinawauma sasa kwa kua wanajua kinachoenda kuwakuta kwani hawana beki ya kumzuia Makacho na washambuliaji wengine, kwanza Makacho anazijua beki zao zote na udhaifu wao kwahiyo hawatamsumbua.” Alijinadi Udeze

Homa ya mashabiki na wapenzi wa mpira wa miguu wilayani kilwa na viunga vyake imezidi kupanda kuelekea katika mchezo wa fainali unataraijwa kupigwa juma mosi ya kwanza ya mwezi wa tisa kwa kuzikutanisha timu zenye majina makubwa katika soka la wilaya ya Kilwa Leceister city toka kilwa Masoko na Black Mob Fc au Makuzi kama wengi wanavyopenda kuuita kutoka Kilwa Kivinje.

Ni mchezo ambao utakua wa kukata na Shoka kwa kua unakutanisha timu kutoka miji miwili tofauti iliyo karibu ambapo mmoja anataka heshima kwa kubakiza ubingwa nyumbani na mwengine anataka heshima ya kupeleka ubingwa nyumbani kwa mara aya pili mfululizo. 

Nani kuibuka na kicheko na nani kuibuka na kilio? Jibu litapatikana siku ya tarehe 2 katika Dimba la ukote mjini Kilwa Kivinje kuanzia majira ya saa kumi jioni ambapo Mundunkolo.Blogspot itakua inakuletea moja kwa moja kitakacho kua kinajili katika mtanange huo.

Previous
Next Post »