KICHANGA CHUI FC MGUU NJE MGUU NDANI LIGI DARAJA LA TATU.



Kilwa,

Timu ya Kichanga chui Fc imefanikiwa kusonga mbele katika mashindano ya ligi daraja la nne ngazi ya wilaya, wilaya ya Kilwa.

Kichanga chui imesonga mbele baada ya kuitupia nje ya mashindano timu ya Al qaeda Fc kutoka Kilwa masoko kwa kuichapa goli moja kwa sifuri katika mchezo uliopigwa jana katika uwanja wa Mwenge (Taifa) mjini Kilwa masoko.

Katika mtannage huo wa kukata na shoka timu zote zilionyesha kucheza mchezo wa kushambuliana na kujihami sana hali iliyopelekea kutopatikana kwa mbabe mpaka muamuzi anapuliza kipyenga kuashiria mapumziko.

 Kipindi cha pili milango ya timu zote iliendelea kuwa migumu licha ya mashambulizi ya mara kwa mara kutoka kwa washambuliaji wa timu zote mbili kabla ya Dickson Ngenje kuiandikia timu yake goli pekee katika dakika za lala salama za mtanage huo.

Kwa matokeo hayo timu ya Al qaeda Fc inaaga mashindano hayo na kuungana na timu za Mihina Fc, Ngome Fc , Tamofa Fc na zinginezo ambazo zimeipa mkono wa buriani timu ambazo zinaendelea na mashindano hayo  yanayotarajiwa kufikia tamati wiki hii.
Mchezaji wa kichanga chui Fc Anzuloon Musa akiwatoka wachezaji wa Al qaeda Fc katika mchezo wa Ligi daraja la nne ngazi ya Wilaya uliopigwa katika uwanja wa Mwenge (Taifa) mjini Kilwa Masoko (Picha na Ally Ruambo)

Timu ya Al qaeda imeyaaga mashindano hayo baada ya kutoka suluhu dhidi ya Mihina Fc, sare ya goli moja kwa moja dhidi ya kichanga chui Fc, kipigo cha goli 3 kwa 2 dhidi ya Kilwa youth soccer academy, kabla ya kukubali kipigo cha goli 1 nunge dhidi ya Kichanga chui Fc.
 
Jumammosi ya wiki hii Kichanga chui Fc itakua uwanjani wakimenyana na Kilwa youth soccer academy ili kumpata bingwa wa kituo cha masoko (Kilwa Kusini) ambaye ataungana na bingwa wa Kilwa kaskazini katika kuiwakilisha wilaya katika ngazi ya Mkoa (ligi daraja la tatu).

Bingwa wa Kilwa Kaskazini atapatikana katika mtange ambao utawakutanisha Al qaeda Fc kutoka Njianne ambaye ni bingwa wa kituo cha Njianne dhidi ya bingwa kutoka kituo cha somanga Casablanca Fc katika mchezo unaotarajiwa kupigwa siku ya ijumaa katika dimba la ukote mjini Kilwa Kivinje.



 Akizungumza na Mundunkolo.Bolgspot.com Naibu katibu mkuu, Chama cha Soka Wilaya ya Kilwa (KILFA) Nd. Ally Liyoka amesema anashukuru mashindano yanaendelea vizuri licha ya kukumbwa na changamoto za hapa na pale hususani swala la ukata kwa vilabu ambavyo vinashiriki ligi hio.

Amesema timu nyingi zimeshindwa kufanya usajili mzuri na maandalizi ya kutosha kwa kua hazina uwezo wa kifedha wa kugharamia gharama hizo hali ambayo imepelekea timu nyingi kushindwa kujitokeza na zilizo jitokeza kushindwa kumudu baadhi ya gharama.

“ukiachana na ukata wa timu lakini pia tunachangamoto katika swala la waamuzi lakini sisi kama viongozi tunajitahidi kulitafutia ufumbuzi.” alisema Bw.Liyoka



Previous
Next Post »